Forums » Presidential campaigns/ Kampeni za urais

BARUA YA WAZI

  • 1 posts
  October 25, 2020 7:20 PM MSK
  KALAMU ISEMAYO MANENO YA ALLY SALEH ALBERTO WA ZANZIBAR BARUA YA WAZI

  Rais Magufuli una saa 72 kuokoa hali Zanzibar

  Assalam aleikum,

  Pole na kampeni ambayo najua kuwa imekuwa ngumu na ya ushindani mkubwa.

  Nimeamua kuandika barua ya wazi kwako kwa sababu kadhaa ukitoa ile ya kuwa sina njia nyengine ya kukufikia hasa kwa udharura kwa jambo niandikalo.

  Sababu ya kwanza ni kutimiza wajibu wangu wa kikatiba kusemea jambo ambalo lina maslahi na nchi.

  Pili ni kutumia uhuru wangu wa kutoa maoni pia kikatiba na tatu ni kuweka rekodi kuwa tupo tuliopaza sauti kuona juu ya jambo hili lakini pia kujaribu kushawishi kuchukuliwa hatua madhubuti juu ya jambo hili nalo ni *KURA YA MAPEMA*.

  Sitaki kuamini ukiwa ni Rais wetu, Amiri Jeshi Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama hujui kinachoendelea kwenye suala zima la hio KURA YA MAPEMA, lakini nimechagua kukupa shaka ya kutokujua ("benefit of doubt").

  Mimi na wengi wetu tunajua na tunakiri suala hili lipo kisheria, Ila shaka yetu na yangu limekosa uhalali na nguvu ya kisheria ("legitimacy and legality"), namna linavyotekelezwa.

  Basi imenitia dhana na fikra kuwa haya yana tokea kukazia kauli ya Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ali kuwa utakuwa mjinga usipotumia dola ulonayo mkononi kubaki katika dola.

  Yeyote yule aliyewaza huu mpango unaoendelea hivi sasa juu ya matumizi ya Kura ya Mapema hakuwaza katika upana na kina.

  Halikadhalika wale watu wanaoshiriki toka mwanzo hadi leo.

  Kama ni mchezo wa "chess" walipanga mezani hatua zao zote mpaka kumteka Malkia, bila ya kutaka kujua kutakuwa na changamoto kadhaa pamoja na kuwa upande wa pili wana mbinu, fikra na mkakati yao.

  Wapangaji wa mkakati wa Kura ya Mapema walichojua wao ni kuweka msingi wa kupata kura 7,000 za kutangulia kwa CCM dhidi ya Wapinzani ACT Wazalendo kwa kura za Okt 27, 2020

  Lakini ACT Wazalendo wanajua kuwa kinachopangwa ni kura 14,000 kwa sababu wapiga kura hao 7,000 wa Oktoba 27 bila ya chembe ya shaka watapiga tena Oktoba 28, 2020.

  ACT wanajua kuwa hio ndio njia peke yake ya hila na ghilba CCM wanaweza kulazimisha ushindi.

  Uchaguzi wote wa kupiga wale wenye haki tu yaani Wazanzibari, uchaguzi wowote wa kura moja mtu mmoja, uchaguzi wowote wa kila kura kuhesabiwa bila kuchezea matokeo... CCM haina nafasi kabisa.

  Mhe Rais, Kuwa CCM haina nafasi ya kushinda Zanzibar sio la leo, Ila kilichobakia ni kauli za " hatutoi nchi", "Tumeshinda kwa bunduki hatotoi kwa vikaratasi," na kauli kama hizo kama kwamba yenye hati miliki ni CCM pekee na Katiba ikifika suala la kushika dola katika Uchaguzi halali huwekwa upande.

  Naelewa sana nikikuambia CCM haiwezi kushinda Zanzibar utakuwa unaumia, maana una wajibu wa kichama kuhakikisha ushindi.

  Ila nakupa tena "benefit of doubt" kuwa hujui kumbe ushindi unaousimamia umeingizwa wizi na magube, lakini ujue huo ndio ukweli.

  Na huko mbele utawajibika kwa litalotokea, tusiume maneno.

  Maana iwapo katika 7,000 wataopiga kura kuna watu pengine nusu yao wanatoka Bara, kwa majina yao na natumai hilo hutalibishia, maanake kama Mwenyekiti wa CCM umesimamia kuvunja Katiba ya Zanzibar ambapo Mpiga Kura ni lazima awe Mzanzibari.

  Na kuna shaka kubwa kuwa watu hao, ili kupata nidhamu ya utii, wanayo kana na vikosi vyetu vya ulinzi, maanake Jeshi limetiwa kwenye tirivyogo la siasa.

  Naweza kuapa asilimia 100 ya majina kutoka Bara tuliobandikiwa vituoni hatuwajui wala hawana anuani mitaani kwetu.

  Kijiji kama Michamvi ambacho hakuna kambi ya Jeshi au kikosi cha aina yoyote kimepata mgao wa wapiga kura za mapema 150

  Lakini pia kama Mwenyekiti itakuwa umesimamia zoezi ambalo kuna wapiga kura wa mapema wa ajira ya Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar au taasisi za Muungano, kwa maslahi ya CCM wataotanzwa kupiga mapema na kwa woga kuitilia CCM bila ridhaa zao na utachangia kuibeba na kuisokota demokrasia upande wa Zanzibar.

  Mhe Rais kwa hali nionavyo Viongozi wetu wa ACT wazi wazi wamehamasisha wanachama na wananchi wajitokeze kwenye KURA YA MAPEMA ya Oktoba 27. Siamini vyombo vyako havijakueleza Hali halisi.

  Wala sitaki kuamini kuwa washauri wako wanakwambia kila kitu kiko sawa na Kura hio itapigwa kama ilivyopangwa na bila athari wala madhara. Usiyaamini.

  UpinzanI umeonewa sana, umedhulumiwa mara nyingi lakini unasema un'yan'ganyi huu hawatauvumilia.

  Maana yake kama kura ya mapema itapigwa kwa vyovyote vile na Kura ilo baki kupigwa basi, tusijidanganye kuwa matokeo yatakuwa na "legality" na "legitimacy."

  Maana yake miaka mitano ya mizozo na mikwamo kwa Zanzibar na hilo ni kwa faida ya nani.

  Naamini ACT haitasusa Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini kutakuwa na faida gani katika hali hii tunayoelekea?

  Mbali ya yote, basi hoja moja ya msingi inaua dhana nzima ya kura ya mapema.

  Nayo ni ile ya hao wanaopiga mapema kuwa kama ni Wazanzibari jee hawatopiga kura Okt 28 kwa Urais wa Zanzibar na dhana ya kua huru kikazi iko wapi?

  Mhe Rais Zanzibar iko pahala pabaya sana na una wajibu wa kuinusuru kuingia katika mgogoro.

  Binafsi sioni kura hio ikisimamishwa kutakuwa na upungufu gani kwa kura ya Oktoba 28.

  Njia yoyote ya kutumia nguvu kulazimisha ipigwe haina mantiki.

  Hoja kwamba ni jambo la kisheria imevurugwa kwa kuingia na wapiga kura wasiotambuliwa na sheria.

  Mhe Rais una saa 72 mikononi mwako na mimi nakuomba, nakusihi uuone wajibu wako huu.

  Mimi na wewe hapa Tuweke U-CCM na U-ACT wangu pembeni...

  Kwa maslahi ya Zanzibar maana uchaguzi utaisha na sisi tunaitaka Zanzibar yetu nzima si vipande vipande.

  Nashukuru kuwa umeisoma barua hii ya wazi kutoka kwa raia wako.

  Ndimi

  Ally Saleh Alberto
  25 Okt, 2020